Story by Our Correspondents –
Tume huru ya uchaguzi na mipaka nchini IEBC imefanya mabadiliko kadhaa ya maafisa wake wa nyanjani na kuwahamishia maeneo mengine ya nchi ili kufanikisha uchaguzi huru na haki.
Naibu Mwenyekiti wa Tume hiyo Juliana Cherera amesema hatua hiyo imetokana na maafisa hao kufanyakazi katika eneo moja kwa mda mrefu na pia itazuia upendeleo katika zoezi zima la uchaguzi mkuu.
Akizungumza na Wanahabari baada ya kuhudhuria kongamano la uzinduzi wa mikakati ya uchaguzi wa amani lililoandaliwa na Shirika la kutetea haki za kibinadamu la HURIA katika eneo la Diani, Cherera amesema taifa hili linahitaji uchaguzi wa amani.
Wakati uo huo amewahakikishia wakenya kwamba Tume ya IEBC imejiandaa vyema kwa uchaguzi mkuu ujao, akisema makamishna na maafisa wa tume hiyo wamepokea mafunzo ya hali ya juu kufanikisha uchaguzi huru na haki.