Tume ya kuajiri walimu nchini TSC, imewahimiza walimu wote kote nchini kuhakikishwa wanajitokeza na kupokea chanjo ya kuzuia maambukizi ya virusi vya Corona.
Afisa mkuu mtendaji katika Tume hiyo amesema Rais Uhuru Kenyatta amekubali kuwaruhusu walimu kupokea chanjo ya kuzuia maambukizi ya Corona kulingana na umri wao ili kuhakikisha virusi hivyo vinadhibitiwa.
Akizungumza katika makao makuu ya baraza la kitaifa la mitihani nchini KNEC kule Nairobi wakati wa kutangazwa kwa matokeo ya mtihani wa KCPE, Nancy amesema huu ni wakati mwafaka wa walimu kujitokeza kupokea chanjo hiyo.
Nancy amesema kufikia sasa zaidi ya walimu 26 wa shule za msingi wamepoteza maisha yao kutokana na maambukizi ya virusi vya Corona, walimu wakuu wakiwa wanane, manaibu walimu wakuu watatu na walimu wengine 15.
Wakati uo huo amewahimiza walimu watakaoteuliwa kusahihisha mtihani wa kidato cha nne wa KCSE kuhakikisha wanapokea chanjo ya kuzuia maambukizi ya Corona sawia na kuzingatia masharti yote ya kudhibiti virusi hivyo kabla ya kuanza kusahihisha mtihani huo.