Mombasa, Kenya, Agosti 10 – Mali ya thamani ya maelfu ya pesa imeteketea baada ya trela moja la kusafirisha mafuta ya petroli kuteketea katika eneo la Kibarani Kaunti ya Mombasa mchana wa leo.
Kulingana na polisi trela hilo lililokuwa likisafirisha mafuta ya petroli, limekabiliwa na hitalafu katika mtambo wake wa injini na likalipuka moto na kuteketea kabisa.
Tukio hilo limekatiza shughuli za uchukuzi katika eneo la Kibarani ambalo ni lango kuu la kuingia Kisiwani Mombasa huku maafisa wa usalama wakiyazuia kwa muda magari kamwe kutoitumia barabara hiyo hadi hali ilipodhibitiwa saa mbili baadaye.
Afisa mkuu wa polisi eneo la Changamwe Daudi Loronyokwe amethibitisha tukio hilo na kusema kwamba kamwe hakuna aliyejeruhiwa kwenye ajali hiyo kwani Dereva na Kondakta wake wamekwepa eneo la mkasa salama.
Hata hivyo, watumizi wa barabara hiyo wametakiwa kuwa waangalifu pindi wanapopitia katika eneo la mkasa akihoji kwamba polisi wameshika doria eneo hilo kwa siku nzima vile vile kuwazuia Wakaazi ambao mara nyingi hukimbilia matrela hayo ili kuteka mafuta pindi yanapokumbwa na hitilafu.