Timu ya voliboli ya watu wanaoishi na ulemavu kutoka Pwani huenda ikakosa kushiriki mashindano ya kitaifa mwezi huu baada ya kukosa mfadhili wa kugharamia safari, malazi na makaazi yao kwa muda wa juma moja Jijini Nairobi.
Mkufunzi wa timu hiyo inayoendeleza shughuli zake katika eneo la Mikindani Kaunti ya Mombasa Bi Ruth Nambuye amesema kwamba licha ya vijana hao walio na vipaji vya hali ya juu katika voliboli kujezatiti katika mazoezi, changamoto ya fedha imetatiza pakubwa jitihada hizo.
Akizungumza katika eneo la Bangladesh huko Mikindani, Bi Nambuye amesema kwamba timu hiyo imekosa sare maalum, vifaa vya kufanyia mazoezi miongoni mwa mahitaji mengine msingi ili kuiwezesha timu hiyo ya pekee ya voliboli ya walemavu katika Kaunti ya Mombasa kuimarisha mchezo wao.
Kwa sasa, Bi Nambuye anawaomba wadhamini na hususan viongozi wa Kaunti ya Mombasa kujitokeza ili kuikimu timu hiyo kwa sare, vifaa vya kuchezea na fedha za kuwawezesha kushiriki michuano hiyo ya voliboli kwa watu wanaoishi na ulemavu Jijini Nairobi.
Michuano hiyo ya voliboli ya walemavu ambayo huchezwa kama wachezaji wameketi chini inaanza tarehe 28 mwezi huu wa Novemba na kukamilika tarehe 3 mwezi Disemba mwaka huu Jijini Niarobi.
Taarifa na Gabriel Mwaganjoni.