Story by Gabriel Mwaganjoni-
Mataifa mengi ya Afrika bado hayajatilia maanani umuhimu wa afya ya jamii hivyo basi yameshindwa kuwekeza mipangilio inayostahili ili kuiboresha afya ya jamii mashinani.
Hayo ni kulingana na mtafiti wa maswala ya kiafya kutoka umoja wa Afrika AU Daktari Herilinda Temba aliyesema ni mataifa 18 pekee yaliyojizatiti na kuweka miundo mbinu ya kuiboresha afya ya jamii japo vile vile mataifa hayo yamekosa kufadhili ipasavyo mipangilio hiyo.
Akilihutubia kongamano la afya la mataifa ya Afrika linaloendelea katika eneo la Nyali kaunti ya Mombasa, Daktari Temba amesema bila ya swala la afya ya jamii kupewa kipau mbele, basi mataifa ya Afrika yatazidi kukumbwa na changamoto ya kuboresha sekta ya afya kwa wananchi.
Daktari Temba hata hivyo amesisitiza umuhimu wa Serikali za mataifa ya Afrika kuungana na kuweka mipangilio inayostahili sawa na kuwaweka wahudumu wa afya ya jamii waliofuzu na ambao watatekeleza majukumu ya kufuatilia kwa kina afya ya jamii mashinani hadi katika familia.
Ni kauli iliyopigiwa upato na Mkuu wa kutengo cha afya ya jamii katika Wizara ya afya nchini Daktari Salim Hussein aliyehoji kwamba ni jukumu la Serikali kuimarisha afya ya jamii mashinani kwa kuwaajiri wahudumu waliyofuzu na watakaojengwa uwezo kutekeleza jukumu hilo.