Taarifa Alphabet Mwadime.
Tamaduni za kale na itikadi potovu zimepelekea visa vingi vya dhuluma dhidi ya mtoto katika Kaunti ya Kilifi kutosuluhishwa kisheria.
Afisa wa maswala ya dharura katika shirika la utetezi wa haki za kibinadamu nchini Haki Afrika, Mathias Hezron Shipetta amesema kwamba itikadi inayoenezwa katika jamii kwamba watoto wadogo huponya virusi pindi mtu anapofanya ngono nao, ni potovu mno na inastahili kuzimwa.
Mtetezi huyo wa haki za kibinadamu ametaka sheria kuchukua mkondo wake kikamilifu ili kumlinda mtoto dhidi ya dhuluma hizo hasa ubakaji.
Wakati uo huo, shirika hilo linafuatilia kesi moja ya ubakaji mjini Kilifi ambapo mtoto wa miaka 2 alibakwa na mwanamume wa umri wa miaka 30 siku moja iliyopita, na hadi sasa mwanamume huyo yuko mafichoni.