Mwenyekiti wa jopo maalum linaloangazia ulanguzi wa binadamu Pwani, George Masese, Masese amesema tamaa ya utajiri ndiyo hunasa vija kwenye uhalifu huo. Picha/ Gabriel Mwaganjoni.
Taarifa na Gabriel Mwaganjoni.
Mombasa, Kenya , Mei 22 – Tamaa ya kupata utajiri wa haraka miongoni mwa vijana katika ukanda wa Pwani ndio chanzo cha biashara haramu ya ulanguzi wa binadamu.
Kulingana na mwenyekiti wa jopo maalum linaloangazia uhalifu huo humu nchini George Masese ni kuwa vijana wengi wanatamani kumiliki mamilioni ya fedha, nyumba kubwa na magari bila ya kuwa na mbinu za kupata mali hizo.
Akizungumza mjini Mombasa katika mkao wa hamasa kuhusu biashara haramu ya ulanguzi wa binadamu, Masese amehoji kuwa ukosefu wa ufahamu, umechangia wakaazi wengi wa eneo hili kuhadaiwa na pesa nyingi pindi wanaposafiri hadi ughaibuni kufanya kazi.
Hata hivyo, Masese amesema utafiti wa jopo hilo umebaini kuwa asilimia kubwa ya wakaazi wa Pwani wanaosafiri katika mataifa ya ughaibuni hupitia madhila mengi ikiwemo kutumiwa katika biashara ya ngono.
“Na unapoenda pale Ng’ambo kwenda kufanya kazi huenndi kufanya kazi ya kibinadamu, kama ni wasichana wanaenda kufanya kazi ya uasherati kwa nguvu na bila kulipwa. Wengine wanaahidiwa pesa nyingi lakini wanaishia kulipwa pesa kidogo ambazo haziwezi kukikimu kimaisha,” amesema Masese.