Zaidi ya watu wanane wamejeruhiwa vibaya jioni ya leo baada ya genge la Vijana wasiyopungua 200 na waliyokuwa wamejihami kwa mapanga, marungu na visu aina ya machete kutekeleza uvamizi katika maeneo ya Bamburi.
Genge hilo limevamia maduka, nyumba za makaazi na watu waliyokuwa wakitoka kazini wakiwajeruhi na kuwaibia mali zao zikiwemo simu za rununu.
Genge hilo linaloaminika kuwa la ‘Wakali kwanza’ baadaye lilivamia duka la Supermarket la Naivas katika eneo la Bamburi na kuwajeruhi wafanyikazi huku likiiba mali na pesa katika duka hilo.
Wanajeshi kutoka katika kambi ya jeshi ya Nyali barracks wameidhinisha oparesheni ya kiusalama katika eneo hilo la Bamburi, maeneo ya Mtopanga, Mwandoni na mengineyo ya Gatuzi hilo dogo la Kisauni.
Maafisa wa usalama wamewaamrisha Wakaazi kusalia ndani ya nyumba kuanzia mwendo wa saa moja usiku wa kuamkia leo huku oparesheni hiyo ya kiusalama ikiendelezwa usiku kucha.
Mmoja wa waathiriwa hao ni mzee Salim Khamis aliyenussurika uvamizi wa genge hilo baada ya kutoroka.
Waliojeruhiwa katika uvamizi huo wamekimbizwa katika hospitali kuu ya ukanda wa Pwani kwa matibabu ya dharura