Mwenyekiti wa tume ya taifa ya ardhi Prof Mohamed Swazuri amemuandikia barua mkuu wa utumishi wa umma Francis Kinyua akitaka kuregeshewa wadhifa wake kama mwenyekiti wa tume hiyo.
Naibu wake Abigael Mbagaya amekuwa akihudumu kama kaimu mwenyekiti wa tume hiyo baada ya Swazuri kufikishwa mahakamani juma lililopita akituhumiwa na kashfa ya ufisadi.
Swazuri anasema bado yeye ni mwenyekiti wa tume hiyo na hatua ya naibu wake kuteuliwa mwenyekiti wa muda imepotoka.
Barua ya Swazuri inajiri huku mashirika ya kijamii yakitoa makataa ya siku 30 kwa makamishna wote wa tume ya taifa ya ardhi kujiuzulu nyadhifa zao. Mashirika hayo yamewalaumu makamishna hao kwa utepetevu pamoja na kujihusisha na ufisadi. Kipindi cha kuhudumu cha tume ya taifa ya ardhi kinakamilika Februari 19 mwaka ujao.
Taarifa na Christine Manyongi.