Story by Mwahoka Mtsumi –
Katibu mkuu wa Chama kutetea maslahi ya walimu nchini KNUT Wilson Sossion amejiuzulu rasmi wadhfa huo aliyoshikilia tangu mwaka wa 2013.
Akizungumza na Wanahabari, Sossion amesema amechukua hatua hiyo ili kuzuia kutokea kwa sintofahamu za kiuongozi ndani ya chama cha KNUT huku akisema wakati wa uongozi wake sekta ya elimu iliimarika pakubwa.
Sossion amesema atasalia kuwa mwanachama muamunifu wa KNUT sawia na kusaidia viongozi wa chama hicho iwapo watahitaji msaada wake huku akisema ana imani kwamba chama cha KNUT kitapiga hatua katika kutetea maslahi ya walimu.
Wakati uo huo ameishinikiza serikali ya kitaifa kutoa malipo ya walimu kwa chama hicho ili kufanikisha shughuli za chama hasa katika kutetea maslahi ya walimu nchini.
Kujiuzulu kwa Sossion kumejiri mda mchache tu kabla ya uchaguzi wa viongozi wakuu wa chama hicho kuandaliwa siku ya Jumamosi ya tarehe 26 mwezi huu katika uwanja wa Ruaraka jijini Nairobi.