Shamrashamra zinaendelea katika shule mbalimbali kaunti ya Mombasa baada ya matokeo ya mtihani wa darasa la nane KCPE kutangazwa huku shule za mitaa ya mabanda katika eneo la Aldina kaunti ya Mombasa zikifanya vyema.
Mkurugenzi mkuu wa shule ya msingi ya kijamii ya Leads katika eneo hilo Elizabeth Nafula amesema kati ya Wanafunzi 68 waliyofanya mtihani huo, wanane wameibuka na alama 400 na zaidi.
Nafula amesema shule hiyo ya kijamii inayowakimu watoto wa zaidi ya familia elfu 20 kutoka mitaa ya mabanda, imezidi kubadilisha hali ya jamii kupitia kwa wanafunzi wanaodhihirisha matumaini makubwa maishani licha ya changamoto.
Nafula amefichua kwamba usimamizi wa shule hiyo uliwekeza katika kuwashauri wanafunzi kutokana na janga la Corona lililowalazimu kusalia nyumbani kwa miezi 9.
Kwa upande wake, mwanafunzi bora zaidi wa shule hiyo aliyepata alama 405 Solomon Chimera amesema alijitahidi kwani alipoteza muda mwingi nyumbani kipindi hicho.