Kamati ya usalama huko Magarini kaunti ya Kilifi imepiga marufuku shughuli zote za uganga wa kienyeji na kuamuru mabango yanayotangaza waganga katika eneo hilo kuondolewa.
Katika kikao na wanahabari huko Marafa mwenyekiti wa kamati hiyo Mbiuki Mutembei amesema yeyote atakayepatikana akiendeleza shughuli za uganga katika eneo hilo atafunguliwa mashataka.
Mbiuki ametoa onyo hilo baada ya kubainika kuwa waganga sawia na wapiga ramli wamechangia pakubwa mauaji ya wazee kwa kutoa taarifa zinazoashiria kwamba wazee hao wanajihusisha na ushirikina.
Hata hivyo, Mbiuki amethibitisha kupungua kwa visa vya mauaji ya wazee kutokana na ushirikiano uliopo kati ya machifu,manaibu wao pamoja na balozi wa nyumba 10 eneo hilo.