Story by: Gabriel Mwaganjoni
Shughuli za uchukuzi zimetatizwa katika barabara kuu ya kutoka Mombasa kuelekea Nairobi baada ya wakaazi wa eneo bunge la Mwatate kaunti ya Taita taveta kuandamana na kuifunga barabara hiyo wakilalamikia kuhangaishwa na wanyamapori.
Wakiongozwa na mzee wa kijiji cha Rong’e eneo bunge hilo Alex Mwawughanga, wakaazi hao wanasema katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita zaidi ya mifugo 350 wameuliwa na Simba huku wenyeji wakiishi kwa hofu ya kuvamiwa na Simba.
Mwawughanga na mkaazi mwenzake Danson Kisombe wamesema juhudi zao za kutaka wanyamapori hao kurudishwa katika mbunga za wanyamapori sawa na wakaazi waliopata hasara kufidiwa zimeambulia patupu.
Hata hivyo, Afisa mkuu wa polisi mjini Voi Bernastein Sharry ameyatibua maandamano hayo bila ya kutoa mwafaka wala suluhu lolote kwa wakaazi hao huku wakaazi wakiapa kukita kambi barabarani hadi pale utata huo utakapotanzuliwa.