Shirika la Search for Common Ground limewahimiza wakaazi wa kaunti ya Mombasa na kote Pwani kuzingatia kikamilifu masharti ya kujikinga dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona.
Afisa wa mipango katika Shirika hilo, Zena Hassan amehoji kwamba ni lazima kila mmoja kuchukua jukumu la kujikinga ili kuzuia msambao wa virusi hivyo katika jamii.
Akizungumza mjini Mombasa wakati wa kupeyana vifaa vya kujikinga na Corona ikiwemo barakao, Zena amesema idadi ya juu ya visa vya maambukizi ya virusi vya Corona vinavyoendelea kunakiliwa nchini imeenza kuwatia hofu wakaazi.
Wakati uo huo ameitaka jamii kujitenga na taarifa ambazo huenda zikawapotosha wengine hasa kuhusu maambukizi ya virusi vya Corona na badala yake kuzingatia kikamilifu masharti ya kujikinga yaliotolewa na Wizara ya Afya nchini.
Hata hivyo kupitia mradi wa Pamoja dhidi ya Corona, Shirika hilo limewagawia wakaazi zaidi ya elfu mbili vifaa vya kujikinga na Corona ikiwemo Barakoa, vieuzi na mitungi ya maji huku liwahimiza vijana kuzingatia amani na usalama.