Story by Gabriel Mwaganjoni-
Shirika la kupambana na dawa za kulevya na pombe haramu nchini NACADA limeweka wazi kwamba visa vya kuteketezwa shule vinavyoshuhudiwa nchini umechangiwa na uraibu wa mihadarati miongoni mwa Wanafunzi.
Afisa mkuu mtendaji wa Shirika hilo Dkt Victor Okioma amesema utafiti wa Shirika hilo kuhusu utumizi wa dawa za kulevya shuleni umebaini wazi kwamba wanafunzi wa hadi miaka 11 tayari wamezama katika uraibu wa dawa hizo.
Akizungumza katika kaunti ya Mombasa, Dkt Okioma amesema mamlaka hiyo inajizatiti kuwashirikisha wanafunzi katika hamasa kuhusu athari za utumizi wa dawa za kulevya ili kuwasaidia wale ambao tayari wameathirika na hali hiyo.
Wakati uo huo, amehimiza ushirikiano kati ya vitengo mbalimbali vya usalama, wadau wa sekta ya elimu na walimu katika kuwakinga wanafunzi dhidi ya utumizi wa dawa za kulevya.