Story by Our Correspondents-
Shirika la kutetea haki za kibinadamu la HURIA limezindua mikakati wa uchaguzi wa amani inayolenga kuhakikisha kaunti tatu za Pwani ikiwemo Kilifi, Mombasa na Kwale zinaandaa uchaguzi huru na haki.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mkurugenzi mkuu wa Shirika hilo Yusuf Lule amesema hatua hiyo itazuia kushuhudiwa kwa siasa za vurugu.
Mwanaharakati huyo ameweka wazi kwamba shirika hilo linashirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo idara ya usalama, Tume ya IEBC, Wanaharakati wa kijamii na Wanahabari kuhakikisha uchaguzi mkuu wa Agosti 9 unazingatia haki.
Akiunga mkono mpango huo, Kamishna wa kaunti ya Kwale Gideon Oyagi amesema kama idara ya usalama tayari imebaini maeneo ambayo yanahitaji usalama zaidi ili kuzuia vurugu za kisiasa wakati wa uchaguzi.
Kwa upande wake Mratibu wa vyama vya kisiasa kanda ya Pwani Ezekiel Obonyo amewaonya wanasiasa dhidi ya kuchangia vurugu za kisiasa, akisema wale watakaopatikana wakiendeleza tabia hiyo watachukuliwa hatua kali za kisheria.