Story by Mwahoka Mtsumi –
Mashirika ya kutetea haki za kibinadamu kanda ya Pwani yamezindua vikao vya hamasa mashinani kuhusu jinsi ya kudhibiti ghasia wakati wa uchaguzi mkuu.
Mashirika hayo yakiongozwa na Shirika la HURIA chini ya Afisa wa nyanjani Mwinyihajj Chamosi yamesema vikao hivyo vitachangia eneo la Pwani kuzidisha uiano wa kijamii na amani.
Chamosi amesema vikao hivyo vimejumuisha viongozi mbalimbali ikiwemo wa kidini, vijana wa bodaboda na hata jamii yenyewe katika juhudi za kuimarisha amani wakati wa uchaguzi mkuu.
Wakati uo huo amedokeza kuwa lengo kuu la kuanzishwa kwa vikao hivyo ni kutathmini maeneo ambayo yanatambulika kwa utovu wa amani na usalama wakati wa uchaguzi na kuishauri jamii kujitenga na vurugu hizo.