Story by Ali Chete
Shirika la kutetea haki za binadamu la Haki Africa limewasilisha ripoti ya uchunguzi wa vurugu za kiusalama zilizoshuhudiwa katika kaunti ya Mombasa kufuatia mihemeko ya kisiasa.
Akizungumza na Wanahabari baada ya kuwasilisha ripot hiyo kwa Tume huru ya uchaguzi na mipaka nchini IEBC katika kaunti ya Mombasa, Mkurugenzi mkuu wa shirika hilo Hussein Khalid amesema ripoti hiyo imejumuisha matokeo yanayohatarisha usalama wa taifa yaliyonakiliwa na makachero wao wa nyanjani.
Khalid amedokeza kwamba watu 14 walijeruhiwa katika vurugu hizo na kuitaka idara ya usalama kufanya uchunguzi wa matokeo hayo.
Mwanaharakati huyo ameitaka idara ya upelelezi, afisi ya mkurugenzi wa mashtaka ya umma, Tume ya uwiano na utangamano wa kitaifa NCIC pamoja na Tume ya IEBC kuvichunguza vyama vya kisiasa vya Wiper na ODM kwani vinahusika na matokeo ya vurugu za kisiasa.
Wakati uo huo ameitaka tume huru ya uchaguzi na mipaka nchini IEBC kutowaidhinisha viongozi ambao wanakabiliwa na kesi mbalimbali za ufisadi na utovu wa nidhamu.