Story by Gabriel Mwaganjoni –
Shirika la kijamii la Clean Mombasa limeishinikiza Wizara ya mazingira na ile ya Serikali ya kaunti ya Mombasa kulifunga jaa la taka la eneo la VOK, gatuzi dogo la Nyali, kaunti ya Mombasa.
Shirika hilo chini ya uongozi wake Daktari Mwinga Chokwe limesema jaa hilo ni lina athari kwa afya ya binadamu kwani liko karibu na makaazi wa watu na ni sharti lifungwe na Serikali ya kaunti ya Mombasa kutafuta eneo mbadala la kutupa taka.
Akizungumza alipoungana na Maafisa wa Serikali ya kitaifa akiwemo Katibu mkuu msimamizi katika Wizara ya mazingira nchini Dkt Mohammed Elmi aliyezuru eneo hilo, Chokwe amesema swala hilo limekuwa tata kwa miaka mingi.
Chokwe amesisitiza kwamba majadiliano hayo kati ya Serikali ya kitaifa na ya kaunti ya Mombasa yanapaswa kusuluhisha uchafuzi huo wa mazingira wa muda mrefu katika eneo hilo.
Dkt Elmi amesema Wizara hiyo ya mazingira inalifuatilia swala hilo hadi lisuluhishwe.