Picha kwa hisani –
Wasimamazi wa shule za msingi kote nchini, wamejitokeza na kudai kuwa shule bado zinakabiliwa na changamoto ya kudhibiti maambukizi ya virusi vya Corona kutokana na baadhi ya shule kukosa kuafikia hatua ya maandalizi.
Wakiongozwa na Mwenyekiti wa Chama cha Walimu wakuu wa shule za msingi nchini Nicholas Gathemia, wamesema shule zinahitaji angalau mara mbili ya nafasi ilioko shuleni ili kuhakikisha usalama wa wanafunzi shuleni dhidi ya Covid-19.
Gathemia amesema zaidi ya wanafunzi milioni 16 wa shule za msingi na upili wanatarajia kurudi shuleni Januari 4, huku shule nyingi zikionekana kukosa kufanya maandalizi yoyote.
Gathemia ameyasema hayo baada ya Kongamano la walimu wakuu wa shule za msingi kule Nairobi, huku akidai kuwa itakuwa changamoto kwa walimu shuleni kudhibiti maambukizi hayo.
Hata hivyo mapema leo, Waziri wa Elimu nchini Profesa George Magoha katika ziara yake ya kielimu kule kaunti ya Muranga, amesema serikali itasambaza shilingi bilioni 19 kwa shule za msingi na upili za umma kabla ya tarehe 4 Januari.