Matayarisho ya sherehe za kumkumbuka shujaa Mekatilili Wa Menza zimekumbwa na dosari baada ya utata kuzuka miongoni mwa viongozi kuhusiana na ni wapi sherehe hizo zitafanyika mwaka huu.
Wazee wa kaya katika eneo la Malindi na Magarini wametofautiana wazi wazi kuhusu sherehe hizo hali inayowaacha wakaazi njia panda wasielewe ni kipi kinaendelea.
Tsuma Nzai ambaye ni mwenyekiti wa kituo cha kitamaduni cha Magarini pamoja na wazee wa kaya wa eneo hilo la Magarini wameshikilia kuwa sherehe hizo zitasalia kusherehekewa eneo la Bungale ambako Shujaa Mekatilili wa Menza alizikwa.
Tsuma ameambia wanahabari kwamba eneo lililozikwa shujaa Mekatilili wa Menza linafaa kukumbukwa na wakenya wote na kupuzilia mbali madai kwamba sherehe hizo zitafanyika kule Shakahola, Chakama.
Naye Mwenyekiti wa muungano wa chama cha Kitamaduni cha MADCA Emmanuel Munyaya amesema kuwa shehere hizo zitafanyika Shakahola kutokana na misingi kwamba eneo la Shakahola ndio eneo ambalo Shujaa huyo alipiga kofi mzungu wakati wa ukoloni.
Fauka ya Hayo Munyaya ameteta kwamba wao kama muungano wa chama cha kitamaduni hawajakuwa na uhusiano mwema baina yao na familia ya Mekatilili wa Menza hivyo kuhamisha sherehe hizo.