Kumekuwepo na shamra shamra katika shule ya msingi ya ‘Leads Academy’ iliyo katika Mtaa wa mabanda wa Jomvu baada ya kutoa mwanafunzi aliyepata alama 415.
Ruth Havera ameibuka mwanafunzi wa kwanza shuleni humo kwa kuzoa alama hizo licha ya shule hiyo kuwalenga watoto wanaoishi katika mitaa ya mabanda.
Mkurugenzi mkuu wa shule hiyo Bi Elizabeth Nafula amewarai wanafunzi hasa wale wasiyobahatika katika jamii kuwekeza zaidi masomoni ili kuibadili hali yao ya maisha.
Bi Nafula amezitaja juhudi za walimu, wazazi na wanafunzi hao kama zinazozidi kuimarisha viwango vya elimu katika shule hiyo.
Katika shule ya msingi ya Amani huko Jomvu Kaunti ya Mombasa mwanafunzi Wisdom Wafula ameibuka na alama 424 katika mtihani wa darasa la nane KCPE wa mwaka huu.
Mwalimu mkuu wa shule hiyo Ali Abdallah ametaja kuridhishwa na kuimarika kwa viwango vya elimu katika shule hiyo ya kila mwaka.
Abdallah amekariri kwamba juhudi za Walimu, Wazazi na mafunzo msingi ya nidhamu kwa Wanafunzi yamewakuza watoto wa shule hio kielimu.
Kulingana na Mwalimu Abdallah juhudi hizo zitaimarishwa zaidi kuhakikisha Wanafunzi wanafanya vyema masomoni ili kujenga msingi wa maisha yao ya mbeleni.
Wakati huo huo, Mwanafunzi Victor Jack Nyawara wa shule ya msingi ya Maryjoy Mjini Mombasa ameibuka miongoni mwa Wanafunzi bora katika Kaunti hiyo kwa kukusanya jumla ya alama 408 huku Mwanafunzi wa mwisho shuleni humo Mbaru Charntel Monje akizoa alama 389 katika mtihani huo.