Story by Bakari Ali-
Mgombea wa ugavana katika kaunti ya Mombasa mfanyabiashara Suleiman Shahbal amemtangaza rasmi Selina Maitha kuwa mgombea mwenza katika kinyang’anyiro hicho.
Katika hafla inayoandaliwa katika eneo la Majaoni eneo bunge la Kisauni kaunti ya Mombasa Shahbal amesema Selina Maitha anatajiriba ya kuwaunganisha wakaazi wa Pwani na kufanikisha ajenda za maendeleo hivyo basi jamii zote katika kaunti ya Mombasa zitakuwa zimejumuisha pamoja.
Selina ambaye ni dadake marehemu Mwanasiasa Karisa Maitha ambaye aliwahikuwa Mbunge wa Kisauni na Waziri wa Serikali za Wilaya miaka ya nyuma kabla ya kufariki kwake mwaka wa 2004 akiwa ziarani nchini Ujerumani.
Shahbal ni mgombea wa kwanza wa ugavana wa Mombasa kumtangaza rasmi mgombea mwenza tayari kwa kipute cha Agosti, 9 huku wagombea wengine wakiwemo Abdulswamad Sharif Nassir ambaye ni Mbunge wa Mvita, Ali Mbogo ambaye ni Mbunge wa Kisauni na Naibu Gavana wa Mombasa Dkt William Kingi wakiwa bado hawajaweka wazi wagombea wenza wao.
Hatua ya Shahbal imeonekana kama ya kuwavunja makali wapinzani wake wa kisiasa Ali Mbogo na William Kingi ambao wameonekana kumezea mate kura za jamii ya Wamijkenda katika kaunti ya Mombasa.