Taarifa na Alphalet Mwadime
Utafiti uliyofanyiwa Kaunti ya Mombasa kuhusiana na mabadiliko ya kiuchumi baada ya huduma za reli ya kisasa SGR umebaini kuwa Kaunti hiyo imesambaratika pakubwa kiuchumi.
Utafiti huo uliyoongozwa na chuo kikuu cha Nairobi ulilenga vigezo vya ajira, usalama, afya na jamii ya Kaunti hiyo hali iliyoashiria kwamba huduma za reli ya kisasa zimeathiri pakubwa vipengele vyote muhimu kwa ukuaji wa jamii zote nchini.
Kulingana na Kiongozi wa utafiti huo Profesa Ken Ogolla,Wafanyikazi wengi katika bandari ya Mombasa, wahudumu katika sekta ya uchukuzi wa masafa marefu kupitia malori ya usafirishaji wa makasha na wale wanaotegemea sekta hiyo kwa mapato wamepoteza ajira.
Utafiti huo uliowashirikisha Mkurugenzi wa chuo kikuu cha Nairobi kitivo cha Mombasa Dakta Sarah Kinyanjui, Joshua Aron, James Njihia na Julius Ogeng’o umebaini kwamba hali ya vijana wengi kupoteza ajira baada ya sekta ya uchukuzi wa malori kusambaratika umepelekea Vijana hao kujitosa katika uhalifu na kutikisika zaidi uchumi wa Kaunti ya Mombasa.
Kwa sasa, wasomi hao wanataka majadiliano ya dharura kuanzishwa ili kuisawazisha hali hiyo kabla ya msukosuko huo wa kiuchumi kudidimiza Kaunti ya Mombasa inayomiliki bandari ya Mombasa na iliyo na raslimali kubwa ya Bahari hindi.