Ni sharti Serikali za mataifa ya Afrika kutekeleza kikamilifu maafikiano ya usawa wa jinsia yaliyopitishwa katika kongamano la kijinsia Jijini Beijing nchini Uchina miaka 25 iliyopita.
Kenya ikiwa mmoja wa wale waliyotia sahihi na kuafikia kutekeleza kikamilifu swala la usawa wa jinsia haijaafikia malengo hayo, huku miswada mbalimbali inayolenga kuafikia usawa wa jinsia nchini ukiwemo mswada wa thuluthi mbili za usawa wa jinsia ukitupiliwa mbali mara tatu mtawalia na bunge la kitaifa.
Mkurugenzi mkuu wa Shirika linaloangazia maswala ya usawa wa jinsia Barani Afrika la FEMNET Bi Memory Kachambwa amesema ni sharti Serikali za mataifa ya Afrika, Umoja wa mataifa ya Afrika (AU) na Umoja wa mataifa (UN) kuyajadili maswala msingi ya uongozi, maendeleo, demokrasia, uchumi, elimu miongoni mwa sekta nyinginezo ambazo mwanamke ana mchango mkubwa.
Akilihutubia kongamano lililowaleta pamoja wadau wa maswala ya usawa wa jinsia na uwakilishi bora wa wanawake Barani Afrika lililokamilika jioni ya leo Jijini Addis Ababa nchini Uhabeshi, Bi Kachambwa ameshikilia kwamba Wanawake hao kamwe hawatarudi nyuma katika jitihada za kupigania usawa wa jinsia.
Ujumbe wa Kenya ukiongozwa na Kinara wa Chama cha NARC Kenya Bi Martha Karua ulihudhuria kongamano hilo la siku tatu Jijini Addis Ababa huku ujumbe huo ukiapa kufanya kila juhudi ili kushinikiza usawa wa jinsia katika maswala msingi nchini yakiwemo uongozi.