Story by Janet Shume–
Shirika la kijamii la Crawn Trust limezihimiza serikali za kaunti hususan ukanda wa Pwani kuhakikisha zinaunda na kutekeleza sheria za kupambana na athari za mabadiliko tabia nchi.
Afisa wa shirika hilo Nobert Nyendere, amesema kufikia sasa ni kaunti 39 pekee kati ya 47 humu nchini ambazo wameweka sheria za kupambana na mabadiliko tabia nchi.
Aidha amesema huenda kaunti ambazo hazijaweka sheria hizo zikakosa kunufaika na fedha zinazolenga maeneo yaliyoathirika pakubwa na mabadiliko tabia nchi.
Akizungumza katika kongamano la wanawake eneo la Diani kaunti ya Kwale, afisa wa shirika hilo Cindy Kobei, amesema kwa sasa wanaendeleza hamasa kwa wanawake wa kaunti hiyo kuhusiana na suala zima la mabadiliko tabia nchi, umuhimu wa kuhudhuria vikao vya umma pamoja na masuala ya bajeti.
Amesema hatua hiyo itachangia pakubwa wanawake kupaza sauti kwa serikali za kaunti kutekeleza miradi inayowafaa ikiwemo ile ya kupambana na athari za mabadiliko tabia nchi.