Serikali ya kitaifa imepata mkopo wa shilingi bilioni 82.7 kutoka Japan unaolenga kutumika katika kuidhinisha miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa daraja na barabara katika kaunti ya Mombasa.
Katika taarifa kwa vyombo vya habari kaimu waziri wa fedha nchini Ukur Yattani, amesema serikali pia imepewa fedha za msaada za shilingi bilioni 6.08 zilizotengwa mahususi kutumiwa katika ujenzi wa barabara ya Dongo Kundu.
Yattani vile vile amesema shilingi bilioni 46.6 katika mkopo huo zitatumika katika ujenzi wa daraja katika kivuko cha feri cha Likoni,ili kuimarisha sekta ya biashara na utalii katika ukanda wa pwani na nchini kwa jumla.
Wakati huo huo amefichua kwamba mkopo huo wa shilingi bilioni 82.7 kutoka Japani utakua na riba ya asilimia 0.1 na utalipwa kwa kipindi cha miaka 28.