Picha Kwa Hisani –
Rais Uhuru Kenyatta amesema Kenya imefaulu kukabiliana na maambukizi ya virusi vya Corona nchini, kwa asilimia 8 kutoka asilimia 13 kuanzia mwezi Juni hadi mwezi Agosti mwaka huu.
Akilihutubia taifa kutoka Ikulu ya Nairobi, Rais Kenyatta amesema kufaulu huko huenda kukapelekea taifa kufikia asilimia 5 ya kudhibiti maambukizi ya virusi vya Corona humu nchini.
Kiongozi wa nchi, amesema baada ya wiki tatu serikali itaandaa mkutano na viongozi mbalimbali wa kidini, wadau wa sekta za kibinafsi na wataalam wa kiafya na serikali za kaunti ili kuangalia mwongozo utakaopelekea taifa hili kukabiliana na janga la Corona kikamilifu.
Hata hivyo amewataka wakenya kueka kanda maswala ya kisiasa na kuishi kwa amani na umoja sawia na kueka kando chuki za kibinafsi ili kuhakikisha taifa hili linaendelea kiuchumi na maendeleo.
Akigusia takwimu za maambukizi ya virusi vya Corona, Kiongozi wa nchi amesema watu 213 wamethibitishwa kuambukizwa virusi hivyo na kupelekea idadi hiyo kuongezeka hadi watu 33,016 katika muda wa saa 24.
Hata hivyo watu 241 waliokuwa wakiugua virusi hivyo wamethibitishwa kupona na kupelekea idadi hiyo kufikia watu 19,296 huku watu watano wakiaga dunia.
Wakati uo huo amewahimiza wakenya kuzingatia masharti ya kiafya katika kudhibiti kusambaa kwa virusi hivyo, licha ya Serikali kupitia Wizara ya Afya nchini kujzatiti katika kukabiliana na maambukizi hayo.