Story by Ali Chete
Mwakilishi wa kike katika kaunti ya Mombasa Asha Hussein Mohamed ameihimiza serikali kuweka mikakati mwafaka ya kukabiliana na janga la mihadarati katika ukanda wa Pwani.
Akizungumza mjini Mombasa Asha amesema serikali imelegeza kamba katika kukabiliana na janga la Mihadarati ambalo limeangamiza idadi kubwa ya vijana katika ukanda wa Pwani na kuitaka kuwajibika zaidi na kuziba mianya ya walanguzi wa dawa za kulevya.
Kiongozi huyo amedokeza kwamba licha ya wadau mbalimbali kujenga vituo vya kurekebishia tabia waraibu wa mihadarati bado idadi ya watumizi wa dawa za kulevya inazidi kuongezeka.
Kauli yake imeungwa mkono na Mkurugenzi mkuu wa Swahili Pot Hub na aliye pia Mwenyekiti wa shirika la msalaba mwekundu tawi la Mombasa Mahamoud Noor aliyesema maara nyingi vijana ambao wako kwenye uraibu wa mihadarati ndio hutumika vibaya na wanasiasa.