Vuguvugu la ‘Okoa Mombasa’ linaloangazia swala la kiuchumi Kaunti ya Mombasa limeitaka Serikali kulikabidhi vuguvugu hilo stakabadhi muhimu kuhusu mradi wa barabara ya reli ya kisasa SGR na ule ya eneo la pili la kuegesha makasha katika Bandari ya Mombasa al-maarufu ‘Container terminal-2’.
Mmoja wa vinara wa vuguvugu hilo na mwenyekiti wa Shirika la utetezi wa haki za kibinadamu MUHURI Khelef Khalifa, amesema miradi hiyo miwili imetekelezwa kwa usiri mkubwa mno licha ya kugharimu mabilioni ya fedha.
Kulingana na Khalifa, mradi wa barabara ya reli ya kisasa kamwe haujaafikia malengo yake ya kiuchumi na kushindwa kulipa deni la mabilioni ya fedha kutoka kwa benki ya kimataifa ya Export inayomilikiwa na Serikali ya Uchina na iliyofadhili mradi huo.
Vile vile licha ya eneo la pili la kuegesha makasha yaani ‘Container terminal-2’ katika bandari ya Mombasa kuwa na manufaa kiuchumi kwa taifa hili, Serikali inanuia kubinafsisha mradi huo kwa kuukabidhi kampuni ya kibinafsi ya uchukuzi wa majini ‘Mediterranean’ ndiposa vugu vugu hilo linataka kupewa stakabadhi zote za kandarasi ya ujenzi, maafikiano ya mikopo yote iliyochukuliwa na matarajio ya pato kutoka kwa miradi hiyo miwili Ili gharama hizo ziwekwe wazi kwa umma.