Mashirika yasiyokuwa ya kiserikali yameihimiza serikali kuu kuhakikisha kuwa wakaazi ambao wamesalia kwenye kambi baada ya kuathirika na mafuriko katika kaunti ya Kilifi wanatafutiwa makao.
Akiongea na waathiriwa takriban 200 baada ya kuwagawia chakula cha msaada katika kambi ya Goshi kule Kakuyuni ,mshirikishi wa shirika lisilokuwa la kiserikali la SORRISI AFRICANI Mauro Stoppa amesema kuwa serikali inastahili kushirikiana na mashirika ya kijamii na yale yasiyokuwa ya kiserikali kuwatafutia wakaazi makao.
Stoppa amehimiza kitengo cha kushughulikia majanga kutoka serikali ya kaunti na ile kuu kuingilia kati kuwasaidia waathiriwa hao anaosema wanahitaji msaada wa chakula, madawa na malazi.
Aidha amepongeza mpango wa serikali kuu wa kuwapa vifaa vya ujenzi waathirwa hao akihoji unafaa kuharakishwa ili wakaazi ambao wangali kwenye kambi wawezeshwe kuendelea na maisha yao.
Taarifa na Charo Banda.