Katibu mkuu msimamizi wa Wizara ya habari, mawasiliano, teknolojia na maswala ya Vijana Bi Nadia Ahmed amesema serikali kuu itawashirikisha vijana katika harakati zote za ubunifu kupitia teknolojia ili wajikimu kimaisha.
Bi Nadia amesema kuwa serikali itajizatiti ili kufanikisha ndoto za vijana ambao wamekumbatia ubunifu kupitia teknolojia na Sanaa, akisema vijana wana uwezo wa kubadili maisha yao iwapo watakumbatia mfumo wa kujibunia ajira.
Akizungumza mjini Mombasa Bi Nadia amewataka vijana kutumia teknolojia ya kisasa na utandawazi katika kubuni miradi ya kibiashara na kujiendeleza kwa kuvumbua mbinu mpya za uwekezaji.
Katibu huyo amesema Maafisa wa kitengo chake watazuru maeneo mbalimbali ya nchi ili kukutana na makundi ya Vijana na kujadili jinsi ya kuboresha uwezo wao katika kubadili hali yao ya maisha.