Story by Mimuh Mohamed –
Rais Uhuru Kenyatta ana mipango ya kukabidhi hati miliki za ardhi kwa wamiliki ardhi katika maeneo mbali mbali ya taifa hili ikiwemo kanda ya pwani, mpango ambao utatekelezwa kabla ya Rais kuondoka mamlakani.
Akithibitisha hilo katika mahojiano ya moja kwa moja kwenye kipindi cha Voroni Enehu katika kituo cha Radio Kaya, Msemaji wa Ikulu ya Rais Kanze Dena Mararo amesema rais Kenyatta amejitahidi kuhakikisha wamiliki ardhi wanapata hati miliki za ardhi zao akitaja zoezi la kutathmini wamiliki halisi wa mashamba kama changamoto inayolemaza utoaji wa hatimiliki.
Kanze amekiri kwamba mradi wa usalama wa chakula wa Galana Kulalu umekosa kufaulu, akisema serikali kupitia mamlaka ya unyunyizaji maji mashamba NIA inashirikiana na wakulima kuhakikisha wanazalisha kiwango cha juu chakula.
Msemaji huyo wa Ikulu aidha amesema ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR umerahisha shughuli za usafirishaji makasha kutoka bandari ya Mombasa hadi maeneo mengine ikiwemo ya nje ya nchi.
Wakati uo huo amekiri kutotimizwa kwa asilimia mia moja ajenda nne kuu za serikali, akitoa hakikisho kwamba serikali itakayochukua usukani baada ya uchaguzi ujao itaendeleza utekelezwaji wa ajenda hizo nne za maendeleo.