Story by Janet Shume –
Wizara ya utalii na wanyamapori nchini imezindua rasmi zoezi la kitaifa la kuhesabu wanyama pori nchini.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo katika hifadhi ya Wanyamapori ya shimba hills kaunti ya Kwale, Waziri wa utalii nchini Najib Balala amesema zoezi hilo litasaidia kutambua idadi kamili ya wanayamapori nchini.
Waziri Balala amezitaka taasisi zinazohusika na uhifadhi wa wanyamapori nchini kutumia sayansi na utafiti katika kuongeza idadi ya wanyamapori ambao wanapatikana kwa uchache nchini kwa lengo la kuinua uchumi wa taifa.
Aidha amesema Wizara ya utalii nchini inalenga kuboresha vivutio vya utalii katika ukanda wa pwani ikiwemo fuo za bahari hindi hasa kaunti za Mombasa, Kilifi na Kwale kwa kuhesabu viumbe vya baharini.
Kwa upande wake Katibu katika Wizara ya utalii nchini Safina Kwekwe amesema zoezi hilo la kuhesabu wanyamapori nchini litawezesha taifa kubaini maeneo yanayopaswa kuzidishwa ulinzi ili kumaliza mzozo kati ya binadama na wanyamapori
Naye mkurugenzi wa Shirika la huduma kwa wanyamapori nchini KWS Brigedia mstaafu John Waweru amesema KWS itaboresha utendakazi wake ikiwemo kutumia teknolojia katika kuhakikisha wanyamapori nchini wanalindwa.
Kaimu mkurugenzi wa taasisi ya utafiti na mafunzo ya wanyamapori Dkt Patrick Omondi amesema zoezi hilo litafanikishwa kwa kutumia ndege maalum sawa na kuwatuma maafisa wa KWS katika mbuga za wanyamapori kuendeleza hesabu hiyo.