Story by Mwahoka Mtsumi –
Serikali imetangaza kuanza awamu ya pili ya utoaji wa dosi ya chanjo ya Corona kwa wakenya kuanzia tarehe 28 mwezi huu na itawalenga wale ambao tayari walipata dosi ya chanjo hiyo mara ya kwanza.
Akizungumza katika kikao cha kila siku cha kutoa takwimu za maambukizi ya Corona, Mkuu wa kitengo kinachosimamia zoezi la utoaji wa chanjo nchini Dkt Willis Akhwale amesema zoezi hilo litaanza na dosi laki moja.
Dkt Willis amesema zoezi hilo la awamu ya pili linatekelezwa kwa kuzingatia muongozo wa Shirika la Afya duniani WHO ili kuzidisha kinga ya mwili ya kupambana na virusi vya Corona.
Kwa upande wake Waziri wa Afya nchini Mutahi Kagwe amesema zoezi hilo litaaza na wahudumu wa afya huku akiwaomba wakenya waliopata dosi ya kwanza ya chanjo ya Corona kuwa na subra.