Picha kwa Hisani –
Serikali imepiga marufuku ndege zote za abiria kutoka taifa la India kuingia humu nchini kwa kipindi cha siku 14.
Waziri wa Afya nchini Mutahi Kagwe ametoa tangazo hilo, akisema litaanza kutekelezwa kikamilifu kuanzia siku ya Jumamosi baada ya kushuhudiwa ongezeko la kasi la maambukizi ya virusi vya Corona na vifo katika mataifa ya kusini mwa bara la Asia.
Waziri Kagwe amesema abiria wote watakaoingia humu nchini kabla ya siku ya Jumamosi watalazimika kufanyiwa vipimo vya lazima vya maambukizi ya virusi vya Corona sawia na kuweka karantini ya lazima ya siku 14.
Kenya imechukua hatua hiyo baada ya taifa la Uingereza, Ufaransa, Hong Kong, Bangladesh, Oman na Singapore kupiga marufuku ndege zote za abiria kutoka taifa la India kuingia katika mataifa hayo.