Serikali imetangaza kuongeza mda wa kafyu hadi tarehe 29 mwezi Mei mwaka huu ili kufanikisha juhudi za kudhibiti msambao wa virusi vya Corona nchini.
Waziri wa usalama wa ndani Dkt Fred Matiang’i ametoa tangazo hilo na kulichapisha rasmi katika gazeti la serikali, akisema masaa ya kafyu kwa kaunti tano zilizofungwa ikiwemo Nairobi, Kiambu, Kajiando, Nakuru na Machakos itaanza saa mbili usiku hadi saa kumi alfajiri.
Waziri Matiangi amesema kaunti zengine nchini zilizosalia masaa ya kafyu yataanza saa nne usiku hadi saa kumi alfajiri huku akiwahimiza wakenya kuzingatia tangazo hilo.
Waziri Matiang’i vile vile ameweka wazi kuwa makongamano ya watu yamepigwa marufuku, sawia na mikutano ya kisiasa hadi Mei, 29 ili kuhakikisha taifa linadhibiti msambao wa virusi vya Corona huku akisisitiza kuwa kila mtu ana jukumu la kuzingatia masharti ya kiafya.
Tangazo hilo la Serikali limejiri baada ya Rais Uhuru Kenyatta mwezi Machi 29 kuongeza mda wa kafyu kwa siku 30 zaidi bila ya kuweka tarehe rasmi ya mwisho wake hali ambayo imepelekea mda huo kuongeza tena hadi Mei, 29.