Picha kwa Hisani –
Rais Uhuru Kenyatta ametangaza kwamba ujenzi unaoendelea wa kituo cha kushughulikia samaki cha Liwatoni kuwa Bandari ya Uvuvi ya kisasa utakamilishwa mapema mwezi Machi mwaka ujao ili kuimarisha uchumi wa rasilimali za baharini.
Kenyatta amesema ujenzi wa bandari ya uvuvi ya Liwatoni utakapokamilika meli zote za uvuvi zinazohudumu katika bahari ya Kenya zitatakiwa kuwasilisha shehena zao katika bandari za Kenya na meli zitakazokiuka agizo hilo zitapokonywa leseni zao.
Kama hatua ya kuongezea samaki thamani, rais Kenyatta ameagiza hazina ya Kitaifa kutoa fedha kwa ujenzi wa kiwanda cha kisasa cha kutayarisha samaki aina ya Jodari katika bandari ya uvuvi ya Liwatoni.
Kufikia mwezi Juni mwaka 2021, wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi imejitolea kutoa mafunzo kwa wavuvi elfu moja wa Kenya ambao wataajiriwa na meli zinazohudumu katika bahari ya Kenya.