Story by Gabriel Mwaganjoni-
Mgombea wa ugavana wa kaunti ya Mombasa kwa tiketi ya chama cha UDA Hassan Omar Sarai amewahakikishia wakaazi wa kaunti hiyo huduma bora pindi watakapomchagua kama gavana wa kaunti hiyo.
Sarai aliyekuwa akijadiliana na wakaazi katika mkao wa bunge la Mwananchi kisiwani Mombasa amesema mkaazi wa Mombasa hahitaji umaarufu wa chama cha kisiasa bali kiongozi muadilifu atakayebadilisha kaunti ya Mombasa kimaendeleo.
Kulingana na Sarai, katika miradi mbalimbali itakayotekelezwa na Serikali kuu na ile ya kaunti wakaazi watanufaika moja kwa moja katika kushiriki ujenzi wa miradi hiyo.
Wakati uo huo, amesema atawekeza mradi wa ujenzi wa nyumba za makaazi kwa wakaazi wa kaunti hiyo watakazoishi kwa bei nafuu, mradi ambao vile vile utamshirikisha mkaazi na mwekezaji wa kaunti ya Mombasa.