Story by Our Correspondents-
Tume ya Elimu ya vyuo vikuu nchini CUE imebatilisha kutambuliwa kwa cheti cha Johnson Sakaja cha Shahada ya Sayansi na usimamizi kutoka chuo kikuu cha Team nchini Uganda huku uchunguzi ukiendelea kuhusu uhalali wa cheti hicho.
Katika barua iliyotumwa kwa vyombo vya habari na kutiwa saini Mwenyekiti wa tume hiyo Prof Chacha Nyaigoti, imeweka wazi kwamba haitambui uhalali wa cheti cha shahada ya masomo ya Sayansi na usimamizi cha Mwanasiasa huyo.
Katika barua hiyo, Tume ya CUE imesema uchunguzi unaoendelea umebainisha wazi kwamba cheti cha Sakaja anayewania ugavana wa kaunti ya Nairobi wakati wa uchaguzi mkuu uhalali wake ni wakutilia shaka.
Tume ya CUE imeiandikia barua tume ya huru ya uchaguzi na mipaka nchini IEBC ikieleza taratibu zilizotumika kufutilia mbali uhalali wa cheti cha Shahada cha Sakaja huku barua hiyo pia ikiwasilishwa mbele ya Wizara ya Elimu nchini.
Haya yamejiri baada ya wakenya kudai kwamba mwanasiasa hayo hana cheti cha shahada cha kumuwezesha kuwania ugavana wa Nairobi hali ambayo ilipelekea Tume ya IEBC kutomuidhinisha na kusababisha kiongozi huyo kuwasilisha kesi Mahakamani kutetea stakabadhi zake za masomo.