Story by Janet Shume –
Naibu Rais Dkt William Ruto amesema njia pekee ya kuokoa uchumi wa taifa hili ni kupitia kuwajenga uwezo wakenya walio chini kiuchumi na hali ambayo itapanua kiwango cha ushuru kinachokusanywa humu nchini.
Katika kikao na Wananahabari baada ya kufanya mkutano wa faragha na wabunge wanaoegemea chama wa UDA katika makaazi yake ya Karen jijini Nairobi, Ruto amesema analenga kuhakikisha nafasi za ajira zinaongezeka humu nchini.
Ruto amesema iwapo uchumi wa nchi utaimarika na wakenya wanaopata kiwango cha chini cha mapato wataboreshwa kibiashara basi taifa hili litazikabili changamoto mbalimbali zinazoshuhudiwa nchini.
Naibu Rais amesisitiza kwamba kuimarika kwa uchumi wa nchi kutasitisha tabia ya serikali kukopa madeni katika mataifa ya ughaibuni ikiwemo Uchina kwani serikali itakuwa na uwezo wa kukusanya ushuru wa kiwango cha juu.
Akigusia swala la maambukizi ya virusi vya Corona, Ruto amesema mkutano huo wa wabunge umeafikia uamuzi wa kusitisha mikutano ya kisiasa nchini ili kuhakikisha wanaangazia mikakati ya kudhibiti maambukizi vya Corona.