Rais Uhuru Kenyatta amewasuta baadhi ya Wabunge wa Pwani, Wafanyikazi wa bandari ya Mombasa na baadhi ya Watetezi wa haki za kibinadamu kwa kueneza uvumi kuhusiana na swala la kubinafsishwa kwa bandari ya Mombasa.
Akihutubu baada ya kuzindua taasisi ya mafunzo ya ubaharia katika chuo cha Bandari Mjini Mombasa, Rais Kenyatta amesema kwamba uvumi huo hauna msingi wowote na hauwezi kulisaidia taifa hili kuimarika kiuchumi kupitia kwa raslimali za Bahari hindi.
Kiongozi wa nchini amesema kwamba kwa ushirikiano na kampuni ya kimataifa ya uchukuzi wa majini ya ‘Mediterranean Shipping Company’, taifa hili litanufaika pakubwa kiuchumi na kubuni nafasi nyingi za ajira hasa kwa mabaharia.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha makuli nchini anayeunga mkono harakati hizo Mohammed Sheria amesema kwamba uvumi huo umewachanganya wakaazi wa pwani akisema hakuna njama za kuuzwa kwa bandari ya Mombasa.
Juma lililopita Wabunge wa Kaunti ya Mombasa, Watetezi wa haki za kibinadamu kutoka Shirika la MUHURI na Wanachama wa Chama cha makuli wanaomuunga mkono katibu wao simon Sang walishikilia kwamba kufuatia ubinafsishaji huo kati ya shilingi bilioni 17 zitakazopatikana Serikali itapata bilioni 2 pekee huku Wakenya wakipoteza nafasi elfu 4 za ajira.
Hata hivyo, kauli ya wadau hao imekinzana na ya Rais Uhuru Kenyatta mapema leo, baada ya kuweka wazi kwamba zaidi na nafasi elfu 2 za ajira zitabuniwa kupitia ushirikiano huo, huku nafasi elfu moja mia tano za mafunzo ya ubaharia katika mataifa ya nje zikibuniwa kwa Wakenya kila mwaka.