Story by Our Correspondents-
Majaji 20 waliopendekezwa na Tume ya huduma za Mahakama nchini JSC kuhudumu katika Mahakama kuu wameapishwa rasmi kuanza majukumu yao.
Akizungumza baada ya kushuhidia kuapishwa kwa majaji hao, Rais William Ruto amewahimiza majaji hao kuhakikisha wanalitumikia taifa hili kwa bidii, uwazi na usawa bila ya kuegemea upande wowote.
Kiongozi wa taifa amewahimiza majaji hao kutokubali kushurutishwa na mtu yeyote katika kutekeleza majukumu yao wala vitisho kwani wameapa kulitumikia taifa hili kwa haki, usawa na uwazi sawia na kuilinda katiba ya nchi.
Majaji hao walioapishwa ni pamoja na Gichohi Patricia, Josephine Mongare, Patricia Nyaundi, Diana Kavedza, Sophie Chirchir, Mwaisha Said, Heston Nyaga na John Chigiti.
Wengine ni pamoja na Peter Mulwa, Lawrence Mugambi, Gregory Mutai, Robert Wananda, Samwel Mukira, Francis Ochieng, Fred Mugambi, Dennis Magare, Florence Macharia, Teresa Achieng na Aleem Visram.
Itakumbukwa kwamba tume ya JSC ilitangaza nafasi hizo za majaji wa mahakama kuu mnamo tarehe 14 mwezi machi.