Story by Our Correspondents
Rais Uhuru Kenyatta amezindua rasmi kampeni ya kitaifa ya ukuaji wa miti kwa kasi kama njia moja wapo ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.
Akizungumza wakati wa halfa hiyo iliyoandaliwa katika Ikulu ya Nairobi, rais Kenyatta amesema hatua hiyo itachangia uimarishaji wa mazingira nchini huku akidokeza kwamba tayari taifa limeanza safari ya kuongeza idadi ya misitu nchini ili kufikia asimilia 30 ya misitu nchini ifikapo mwaka wa 2050.
Kiongozi wa taifa amehimiza umuhimu wa wakenya kuhakikisha wanakumbatia mpango wa upanzi wa miti nchini ili kuboresha mazingira sawa na kuchangia chemichemi za maji ili kukabiliana na kiangazi kikali kinachochangiwa na mabadiliko ya tabia nchi.
Wakati uo huo, Rais Kenyatta amedokeza kwamba serikali imeanzisha hazina ya kukuza miti kimataifa kwa ushirikiano na wadau mbalimbali ikiwemo Multi partner Trust Fund.