Story by Janet Shume –
Rais Uhuru Kenyatta amewasihi maafisa wa usalama kutafuta ushauri nasaha wanapokumbwa na changamoto za maisha na wala sio kutumia vibaya silaha zao kuwadhuru watu wasio na hatia.
Akizungumza wakati wa hafla ya kufuzu kwa makurutu wa kitengo cha GSU huko Embakasi jijini Nairobi, Rais Kenyatta amesema tatizo la afya ya akili linaweza kukabiliwa ipasavyo kupitia ushauri nasaha.
Kiongozi wa taifa amesema japo kuna baadhi ya wakenya wanaokabiliwa na changamoto za msongo wa mawazo na zile za kimaisha ikiwemo maafisa wa usalama ni vyema iwapo watu hao watajitokeza na kueleza shida zao ili zitatuliwe.
Rais Kenyatta amekashfu vitendo ambavyo vimekuwa vikitekelezwa na baadhi ya maafisa wa usalama ikiwemo kusababisha mauaji, akiwataka maafisa wa usalama kuzungumza na wakubwa wao ili kuzikabilia changamoto hizo.
Kwa upande wake Waziri wa usalama wa ndani Dkt Fred Matiangi amewataja maafisa hao wa usalama 5,112 waliofuzu kama watakaosaidia katika kuimarisha kwa usalama wa taifa hili.