Rais Uhuru Kenyatta, amewaongoza wakenya katika halfa ya uzinduzi rasmi wa ripoti ya BBI huku akiwahimiza kuisoma kwa kina ripoti hiyo kabla ya kufanya maamuzi ya kuiunga mkono au la.
Katika hotuba yake kwa wakenya wakati wa uzinduzi huo katika ukumbi wa Bomas kule Nairobi, Rais Kenyatta amepasua mbariki kuhusu uhusiano wake wa kisiasa na Kinara wa Chama cha ODM Raila Odinga, akisema lengo kuu ni kuwaunganisha wakenya.
Kiongozi wa nchi, ameonekana kuunga mkono mchakato wa BBI, akiwataka wakenya kujitokeza na kuisoma ripoti hiyo kisha kuipitisha ili kubadilisha maswala kadhaa ambayo yameonekana kutafanikisha uongozi.
Hata hivyo, amesema ni kupitia kuboreshwa uchumi wa nchi ndipo changamoto zinazowakumba wakenya hasa vijana zitapata suluhu la kudumu huku akiwataka viongozi kukomesha tabia ya kuwagonganyisha vijana kwa malengo yao binafsi.
Akigusia swala la siasa la mwaka 2022, Rais Kenyatta amewataka viongozi kuwa na subra na kueka kando siasa na kuangazia maswala yatakayowanufaisha wakenya, akisema ni mapema mno kuangazia siasa.
Kwa upande wake Naibu Rais Dkt William Ruto amehimiza kujumuishwa kwa wakenya wote katika kuchangia mabadiliko kwenye Katiba ya nchi, akisema mapendekezo ya wakenya nafaa kujumuishwa katika Ripoti hiyo huku akionekana kuikosoa ripoti hiyo kwa kudai kutoangazia idara ya Mahakama.
Naye Kinara wa Chama cha ODM Raila Odinga, amewataka wakenya kueka kanda tofauti zao na badala yake kuungana kwa malengo ya kufanikisha maswala mchakato wa BBI, huku akisema huu sio wakati mwafaka wa kuzungumza siasa za mwaka 2022.