Picha kwa Hisani –
Rais Uhuru Kenyatta ameweka wazi kuwa shughuli za masomo nchini zitasalia kufungwa hadi mikakati mwafaka ya kiafya kwa wanafunzi na walimu itakapoafikiwa.
Akizungumza baada ya kupokea ripoti ya Covid-19 kutoka Waziri wa Afya nchini katika Kongamano la kuangazia ufanisi uliopigwa kudhibiti janga la Corona, Rais Kenyatta amesema kalenda ya masomo itatolewa na Wizara ya Elimu nchini baada ya kuafikia mikakati mwafaka.
Hata hivyo Kiongozi wa nchi, ameongeza muda wa Kafyu kwa siku 60 zaidi kuanzia saa tano usiku hadi saa kumi alfajiri huku maeneo ya kujivinjira, baa na hoteli zikifungwa saa nne usiku.
Rais Kenyatta pia ameongeza kiwango cha idadi ya waumini katika nyumba za ibada kutoka ya watu 100 hadi thuluthi moja huku ikiongeza idadi ya watu wanaofaa kuhudhuria halfa za mazishi na harusi kwa idadi ya watu 200.
Wakati uo huo amedokeza kuwa virusi vya Corona nchini vimeshuka kwa asilimia 4.4 katika kipindi cha mwezi mmoja kutoka asilimia 5 kati ya mwezi Juni na Julai mwaka huu.