Picha kwa Hisani –
Rais Uhuru Kenyatta ametia saini kuwa sheria mswada wa ugavi wa mapato kwa kaunti wa mwaka 2020/2021 hatua inayotoa nafasi kwa serikali zote za kaunti kupokea mgao wa fedha za mwaka huu wa kifedha.
Sheria hiyo mpya inaruhusu kutolewa kwa shilingi bilioni 369.87 katika mwaka huu unaoendelea wa kifedha kwa kaunti , na fedha hizo zinajumuisha shilingi billion 316.5 ambazo ni jumla ya mgao sawa kwa kila kaunti na shilingi bilioni 13.73 zitakazotolewa kama ufadhili kwa kaunti kutoka kwa Serikali ya Kitaifa.
Vile vile, fedha hizo zinajumuisha shilingi bilioni 9.43 kutoka kwa hazina ya udumishaji barabara na ushuru wa mafuta ikiwemo Mikopo na ufadhili wa shilingi bilioni 30.2.
Mswada huo umewasilishwa kwa rais Kenyatta katika ikulu ya Nairobi na spika wa bunge la seneti Ken Lusaka,hafla ya kutiwa saini imehudhuriwa na spika wa bunge la kitaifa Justine muturi na waziri wa fedha nchini Ukur Yattani.
Wengine waliokuwepo ni kiongozi wa wengi katika Bunge la Seneti Samuel Poghisio na mwenzake wa Bunge la kitaifa Amos Kimunya,makarani wa mabunge yote mawili Jeremiah Nyegenye na Michael Sialai ,wakili mkuu wa serikali Ken Ogeto na Naibu mshauri mkuu wa Ikulu Njee Muturi.