Story by Our Correspondents –
Rais Uhuru Kenyatta ametia saini kuwa sheria, mswada wa marekebisho ya sheria ya vyama vya kisiasa ya mwaka wa 2021 baada ya bunge la seneti kupiga kura kwa kauli moja na kuupitisha mswada huo siku ya Jumatano usiku.
Sheria hiyo inampa nguvu Msajili wa vyama vya kisiasa nchini, kuthibitisha orodha ya wanachama wa vyama vya kisiasa na kanuni za uteuzi wa wagombea pamoja na kuimarisha usimamizi wa vyama vya kisiasa na demokrasia nchini.
Mswada huo pia unalenga kuimarisha majukumu ya vyama vya kisiasa na jinsi miungano inavyofaa kugawanya fedha kutoka kwa hazina ya vyama vya kisiasa sawa na kuainisha kazi za vyama vya kisiasa.
Hata hivyo mkuu wa sheria nchini Paul Kihara, Spika wa bunge la Seneti Ken Lusaka, na mwezake wa bunge la Kitaifa Justine Muturi, Kiongozi wa wengi katika bunge la Seneti Samuel Poghisio na mwenzake wa bunge la kitaifa Amos Kimunya ni kati ya viongozi walioshuhudia Rais Kenyatta akitia saini mswada huo kuwa sheria.