Picha kwa hisani –
Rais Uhuru Kenyatta amefungua rasmi bandari ya Lamu ambayo inatarajiwa kubuni ajira zaidi elfu 143 kwa wakaazi wa Pwani sawia na kuimarisha shuhuli za uchukuzi, biashara na uchumi katika kanda ya Afrika mashariki na kati.
Akilitubia taifa baada kushuhudia upakuaji wa shehena za mizigo kutoka kwa meli mbili kubwa zilizotia nanga katika bandari hiyo, Rais Kenyatta amewakaribisha wawekezaji kuimarisha uchumi wa nchi kupitia bandari hiyo.
Kiongozi wa taifa amewahimiza wasimasimizi wa mradi huo kuhakikisha wanawapa kipau mbele vijana wa kaunti ya Lamu kwa ajira sawia na kuwatambua vijana kutoka maeneo mengine ya nchi.
Wakati uo huo amewaomba wakaazi wa kaunti ya Lamu kushirikiana na maafisa wa usalama katika kuimarisha usalama kaunti hiyo sawia na kuwafichua magaidi kwa maafisa wa usalama ili kukabiliwa kikamilifu.
Kwa upande wake Gavana wa Lamu Fahim Twaha ameiomba serikali kupitia Rais Kenyatta kuiongezea fedha za zaidi serikali ya kaunti ya Lamu ili kuekeza katika ujenzi wa makaazi ya kisasa na kuwavutie wawekezaji.
Hata hivyo wakaazi wa Lamu walioshuhudia ufunguzi huo wa bandari ya Lamu wameipongeza serikali kwa kuanzisha mradi huo mkubwa, wakisema wakaazi wa kaunti ya Lamu wataimarika zaidi kibiashara na uchumi.
Mradi huo wa bandari ya Lamu imeigharimu serikali shilingi bilioni 310 na tayari maeneo mawili ya kuegesha meli kubwa yamekamilikia ili kufanikisha shuhuli za uchukuzi katika bandari hiyo.